PINGO’S FORUM
SHERIA YA NDOA
Pingo’s Forum na VETAID na kufadhiliwa na DFID
SEHEMU YA KWANZA
MAANA YA NDOA
Kufuatana na sheria ya ndoa ya
mwaka 1971, Ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke unaokusudiwa
kudumu kwa muda wa maisha yao.
AINA ZA NDOA;
Kuna aina mbili za ndoa ;
i) ndoa ya mke mmoja, hii ni
ndoa ambapo mwanaume ana mke mmoja tu.
ii] ndoa ya wake wengi, hii ni
ndoa ambayo mwanaume ana wake zaidi ya mmoja.
Ndoa itokanayo na dhana ya
ndoa; hii ni ndoa ambayo mwanamke na mwanaume wamekaa pamoja ndani ya
nyumba kama mke na mme kwa muda wa miaka miwili na kuendelea na wote wakapata
hadhi ya kuwa wanandoa.
Je ni vipengele gani vya
kuzingatia ili wanaotaka kufunga ndoa wakubaliwe kisheria kufunga ndoa yao?
(a) NI LAZIMA MUUNGANO UWE WA HIARI:
Mume na
mke wawe wameamua kuishi pamoja kwa ridhaa yao wenyewe. Hii inamaanisha kusiwe
na kulazimishwa, kuhadaiwa kwa aina yoyote kwani muungano kama huo utakuwa
batili kisheria. Ni kosa la jinai kushiriki katika shughuli ya ndoa ambayo
mmoja wapo au wote wamelazimishwa kufunga ndoa.
(b) MUUNGANO UWE NI KATI YA
MWANAMKE NA MWANAMUME:
Muungano
wa watu wa jinsia moja hata kama ni wa hiari muungano huo hautambuliki
kisheria. Pia mtu huhesabika mwanamke au mwanaume kutokana na sehemu za siri
alizozaliwa nazo na siyo alizozipata baadaye. Jamii inachukulia kuwa ndoa ni
njia pekee ya kujipanua. Upanukaji huku ni kwa kuzaa watoto. Kwa hali hiyo ili
kupata watoto ni lazima ndoa iwe kati ya mwanaume na mwanamke.
(c) MUUNGANO HUO UWE
UNAKUSUDIWA KUWA WA KUDUMU:
Pamoja na
kuwa mwanamke na mwanaume wameamua kuishi pamoja kwa hiari yao lakini siyo
kwa kudumu muungano huo hautambuliki kisheria kama ndoa.
Muungano ni lazima uwe wa kudumu maisha yote au kama mmoja wao amefariki au
kama ndoa imekumbwa na matatizo na mahakama ikaona ni bora kutoa talaka kwa
yeyote aliyefika kulalamika.
(d) WAFUNGA NDOA WASIWE MAHARIMU:
Maharimu ni watu walio na
mahusiano ya karibu ya damu au kindugu.
Wawili wanaoamua kufunga ndoa
wasiwe na uhusiano wa karibu kindugu. Inakatazwa katika kifungu cha 14
cha Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 mtu kuoa au kuolewa na mzazi wake,
mtoto au mjukuu wake, kama ni dada yake, mama au shangazi au baba wa mjomba
wake, baba au mama wa kambo na mwanaye aliyemfanya kuwa mtoto wake (adopted
child).
(e) WAFUNGA NDOA WAWE WAMETIMIZA UMRI UNAOKUBALIKA KISHERIA:
Mwanamke na mwanaume wawe
wametimiza miaka 18 ili kufunga ndoa. Hata hivyo mwanamke anaweza kuolewa akiwa
na umri wa chini ya miaka
18
lakini sio chini ya miaka 15 kama atapata idhini ambayo hutolewa na baba na
kama hayupo ni mama au kama wote wamefariki idhini itatolewa na mlezi wa binti
huyo. Kama wote wamefariki basi hatahitaji idhini. Kuna wakati katika mazingira
fulani mahakama inaweza kutoa idhini kwa binti kuolewa akiwa na miaka 14 lakini
si chini ya hapa ikiwa ataonekana kwa mfano ana mimba. Pia mwanaume anaweza
kuruhusiwa na mahakama kuoa akiwa na umri wa miaka chini ya 18 lakini lakini si
chini ya 16 kama ataonyesha kuelewa jukumu lake kama mtu mzima. Lakini hii ni
pale ambapo kuna tatizo kama la kumpa msichana mimba ndipo mahakama inaweza
ikatoa idhini. Katika ombi la kuoa la SHABIRI A. M. VIRJI (1971) HCD NO. 407 la
Mahakama Kuu ya Tanzania, mwombaji alikuwa na miaka 16 lakini alimpa mimba
binti wa miaka 18. Mahakama katika kuchunguza ombi la mvulana la kuoa ilitoa
kibali kwa sababu wote wawili walipendana sana na wazazi wao hawakuwa na
kipingamizi cha wao kuoana.
(f) KUSIWE NA NDOA
INAYOENDELEA:
Kama mwanamke ana ndoa inayoendelea
na inatambulika kisheria haruhusiwi kufunga ndoa nyingine (Polyandry).
Kadhalika kama mwanaume ana ndoa ya mke mmoja au kama ni mwislamu ana wake
wanne tayari hataruhusiwa kufunga tena ndoa.
(g) KUSIWE NA KIPNGAMIZI:
Kama ndoa imezuiwa na Mahakama
au halmashauri ya usuluhishi kutokana na uwezo zilizopewa na ndoa ikaendelea
kufungwa kabla ya wenye kupeleka kipingamizi hawajasikilizwa au Mahakama
imeshaamua ndoa hiyo isifungwe basi ndoa hiyo itakuwa ni batili.
(h) MFUNGISHAJI NDOA KUTOKUWA NA MAMLAKA:
Kama wanaofunga ndoa wanajua
wazi kuwa anayewafungisha ndoa hana mamlaka hayo na kwa makusudu wakakubali
awafungishe ndoa basi ndoa hiyo itakuwa ni batili. Mfungishaji ndoa ili kuwa na
mamlaka anapaswa kusajiliwa na Msajili Mkuu wa Ndoa na kupewa leseni ya kufungisha
ndoa.
(i) KUTOKUWEPO KWA WAFUNGA
NDOA:
Kama ndoa imefungwa bila ya
wafunga ndoa wote kuwepo basi ndoa hiyo haitambukuliki kisheria. Hata hivyo
sheria inaruhusu ndoa kufungwa ikiwa mmoja wa wafunga ndoa hayupo, Kama mfunga
ndoa ambaye hayupo amewakilishwa na mtu ambaye alikuwepo wakati mfunga ndoa
hayupo, alipotoa ridhaa yake ya kuoa au kuolewa.
(j) MASHAHIDI WA NDOA:
Ili ndoa itambulike kisheria
ni lazima ishuhudiwe na mashahidi wasiopungua wawili ambao wanaruhusiwa
kisheria yaani umri wao usipungue miaka 18 na wafahamu kinachosemwa na
kutendeka wakati wa kufunga ndoa.
(k) KUWA KATIKA EDA:
Eda ni kipindi cha kukaa ndani
kinachotolewa kwa mwanamke wa kiislamu aliyeachika katika ndoa au aliyefiwa na
mumewe, ili taratibu fulani za kidini zifanyike.
Kama mwanamke ambaye ndoa
ilifungwa Kiislamu anaolewa wakati wa kipindi cha Eda hakijaisha basi
ndoa
hiyo ni batili. Lakini mfaruku au mtalikiwa awe anafuata dini ya Kiislamu. Kama
atabadili dini baada ya kufiwa au kupewa talaka masharti ya Eda hayatambana.
SEHEMU YA PILI
AINA ZA UFUNGAJI WA NDOA NA TARATIBU ZA KUFUATA:
TAARIFA YA NIA YA KUOANA:
Kwanza kama mwanamke na
mwanaume wanataka kufunga ndoa ni wajibu taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe
kwa mfungishaji ndoa siku 21 kabla ya siku ya kufunga ndoa. Taarifa hiyo
ionyeshe mambo yafuatayo:-
(i) Majina kamili na umri wa
hao wanaotaka kuoana.
(ii) Uthibitisho kwamba hakuna
kipingamizi dhidi ya hiyo ndoa wanayotarajia kufunga.
(iii) Majina kamili ya wazazi
wao na sehemu
wanakoishi.
(iv) Hadhi ya wafunga ndoa.
Yaani kama ni
mwanamke ifahamike kama
hajaolewa,
ametalakiwa
au ni mjane na mwanaume pia anapaswa kama hajaoa, au ana mke
/ wake
wengine (Hii ni kwa ndoa za kiserikali na Kiislamuu) au kama ametaliki.
(v) Kama muolewaji ana umri chini ya miaka 18, jina la
mtu aliyetoa idhini ya yeye kuolewa kama yupo ionyeshwe.
(vi) Kama
ni ndoa ya Kiserikali au Kiislamuu
hapana
budi kueleza kama ndoa ni ya wake wengi au inatazamiwa kuwa ya wake wengi,
majina ya wake waliopo yatajwe. Pia katika fungu hili kama mtu anataka ndoa iwe
ya mke mmoja anapaswa kueleza. Baada ya taarifa yenye maelezo haya kufikishwa
kwa mfungishaji ndoa yeye anawajibika kutangaza hii nia ya kufunga ndoa. Sababu
ya kufanya hivyo ni ili kama kuna mwenye kipinganizi na ndoa hiyo atoe taarifa.
Matangazo haya hutolewa kama ndoa inatarajiwa kufungwa kidini, sehemu za ibada.
Kama ni ndoa ya Kiserikali tangazo litabandikwa nje ya ofisi ya msajili wa Ndoa
ambaye ni Mkuu wa Wilaya. Vipingamizi vya ndoa viko vya aina mbili, cha kwanza
ni kile cha kisheria yaani kama ndoa itakayofungwa itakuwa batili. Kipingamizi
cha pili ni kama muoaji ana mke au wake wengine tayari, hivyo mke au wake
wanaweza kutoa kipingamizi kama uwezo 0
wa muoaji kifedha ni mdogo kiasi kwamba kuongeza mke
mwingine kutazidisha taabu.
Mfungishaji
ndoa anapopokea taarifa ya kupinga ndoa isifungwe, ataipeleka taarifa hiyo
kwenye Baraza la Usuluhishi la Ndoa. Huko aliyewekewa kipingamizi na aliyeweka
wataitwa na kila mmoja atajieleza. Baada ya kusikiliza pande zote Baraza lina
uwezo wa kuamua ndoa hiyo ifungwe au isifungwe na mfungishaji ndoa atafuata
uamuzi wa baraza. Kama mtu atatoa kipingamizi cha uongo na ikithibitika hivyo,
adhabu yake anaweza kufungwa kifungo kisichozidi miaka mitatu. Baada ya
kipengele hiki kutimizwa ndoa inaweza kufungwa.
AINA ZA NDOA:
Kuna aina mbili za ndoa:
(a) NDOA YA MKE MMOJA:
Huu ni
muungano unaoruhusu mwanaume kuoa si zaidi ya mke mmoja. Mfano: Ndoa ya
Kikristo.
(b) NDOA ZA ZAIDI YA MKE MMOJA:
Huu ni
muungano unaoruhusu mwanaume kuoa mke zaidi ya mmoja. Mfano, ndoa za Kiislamu
na ndoa za kimila.
Sheria ya ndoa inatambua aina 3 za ufungaji wa ndoa yaani
kiserikali, kidini na kimila.
Ndoa hizo
zaweza kufungwa kwa kufuata taratibu za kidini au za kiserikali. Utaratibu huo
utafuata au kuzingatia kama wanandoa ni waumini wa dhehebu Fulani au la.
(a) NDOA YA KIDINI:
Ndoa hii
hufungwa kwa mujibu wa taratibu ya dini husika. Ni lazima masharti yote
yatimizwe kisheria na taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe na ndoa ifungiwe
mahali pa wazi panapokubalika kisheria na mfungishaji awe na mamlaka hayo
kisheria.
(b) NDOA YA KISERIKALI:
Ndoa hii
hufungwa mbele ya Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Msajili wa Ndoa. Ndoa itafungiwa
katika ofisi ya Msajili au mahali pengine popote palipotajwa katika leseni yake
ya kufungisha ndoa.
(c ) NDOA YA KIMILA:
Ndoa
inaweza kufungwa kimila iwapo mmoja wa wafunga ndoa au wote wawili wanafuata
sheria za mila za kabila fulani. Mwandishi wa ndoa za kimila
ni Katibu Tarafa. Ndoa ya kimila hufungishwa na mtu
anayetambulika kimila kuwa ana uwezo huo. Ni muhimu sana Katibu Tarafa
kuhudhuria kwenye ufungishaji huo wa ndoa kwani ndiye atakayehusika na kuleta
vyeti vya ndoa kutoka kwa msajili.
SEHEMU YA
TATU
UFUNGAJI NDOA NJE YA NCHI:
Kifungu
cha 8 cha sheria kinampa mamlaka Waziri wa
Sheria kuteua baadhi ya maofisa ubalozi kuwa wasajili wa ndoa. Ni lazima
msajili aridhike kuwa masharti yote yametimizwa ndipo afungishe ndoa. Kuna
masharti ya nyongeza kama angalau mmoja wa wafunga ndoa awe ni Mtanzania. Pia
kama mmoja wa wafunga ndoa si mtanzania ni lazima Msajili aridhike kuwa ndoa
inayokusudiwa kufungwa itatambulika kisheria katika nchi ambayo huyo mmoja wa
wafunga ndoa ni mkazi. Utaratibu unaotumika kufungisha ndoa hizi ni sawa na ule
unaotumika katika kufungisha ndoa za kiserikali.
DHANA YA KUCHUKULIA NDOA:
Kuna dhana inayokanushika
(rebuttable
presumption) kuwa mwanaume na
mwanamke wakiishi pamoja kwa miaka miwili au zaidi huchukuliwa kuwa ni mke na
mume mbele ya sheria japokuwa hawakuwahi kufunga ndoa. Dhana hii imeelezwa
katika kifungu cha 160 cha Sheria ya Ndoa.
Ili
dhana hii iwepo ni lazima yafuatayo yathibitishwe.
(i) Lazima ithibitike kwamba
mwanamke na
mwanamume wameishi pamoja kwa
muda wa miaka 2 au zaidi kwa mfululizo.
(ii) Lazima pia ithibitike
kuwa umma
unaowazunguka unawachukulia na
kuwapa heshima kama mke na
mume.
(iii) Lazima ithibitishwe kuwa
watu hao
walikuwa na uwezo wa kuwa mke
na mume
wakati walipoanza kuishi
pamoja kama umri ulikubalika kisheria.
(iv) Ni lazima pia
ithibitishwe kuwa kati ya hao
wawili au
wote hakuna aliye na ndoa
inayoendelea.
NDOA BATILIFU NA SABABU
ZINAZOWEZA KUIFANYA NDOA KUWA BATILIFU:
Ndoa
batilifu ni ndoa ambayo itachukuliwa kisheria kuwa ni ndoa halali hadi hapo
amri ya kuivunja itakapotolewa. Ndoa batilifu ni halali kama
ndoa nyingine isipokuwa ina kasoro fulani. Wanandoa katika ndoa hii wana haki
na wajibu sawa kama ilivyo katika ndoa nyingine zisizo na kasoro. Kadhalika
watoto waliozaliwa katika ndoa ya namna hii ni halali na wana haki zote
kisheria.
NI VITU GANI VINAFANYA NDOA KUWA BATILIFU:
1. MARADHI YA ZINAA:
Kama
wakati wa kufunga ndoa mmoja wa wafunga ndoa alikuwa na maradhi ya zinaa na
yule asiye na Ugonjwa kama wakati wa kufunga ndoa alikuwa hajui lolote anaweza
kulalamika mahakamani na ndoa ikavunjwa.
2. KUKATAA KWA MAKUSUDI KUITIMILIZA NDOA:
Kama
baada ya kufunga ndoa mmoja wa wafunga ndoa atakataa kuitimiliza ndoa
anayekataliwa ana haki ya kuiomba mahakama kuvunja ndoa hiyo. Maingiliano
yanayotambulika kisheria ni yale yanayofanyika siku ya ndoa na kuendelea na
siyo kabla ya ndoa. Kukataa kuitimiliza ndoa kunakuwa sababu ya kubatilisha
ndoa ikiwa mwenye kukataa hana sababu yoyote ya msingi na mwenye kukataliwa
ametumia kila mbinu kumshawishi aliyekataa lakini ikashindikana kufanya tendo
la ndoa.
3. MIMBA YA MWANAUME MWINGINE:
Kama
wakati wa kufunga ndoa mke atathibitika ana mimba aliyopata kwa mwanamume
mwingine, mume
anaweza kuiomba mahakama ivunje ndoa hiyo. Kama
itathibitika kuwa mume alijua hivyo hali wakati wa kufunga ndoa, lalamiko lake
halitasikilizwa.
4. WAZIMU AU KIFAFA CHA VIPINDI:
Mmoja wa
wafunga ndoa kama ana wazimu au kifafa cha kurudia rudia na mwenzake alikuwa
hajui hilo hali wakati wa kufunga ndoa, atakuwa na haki ya kuiomba mahakama
kuivunja ndoa hiyo. Ieleweke kuwa Ugonjwa ni lazima uwe unarudia rudia na siyo
mtu awe aliugua na akapona.
5. KUSHINDWA KUITIMILIZA NDOA:
Kama
mmoja wa wafunga ndoa atashindwa kuitimiliza ndoa basi ndoa hiyo inaweza
kubatilishwa. Kwa mwanaume kama anashindwa kuitimiliza ndoa kwa sababu ya
kukosa nguvu za kiume basi ana haki ya kuiomba mahakama kuibatilisha ndoa. Ili
kukosa nguvu za kiume kuwe sababu ya kubatilisha ndoa ni lazima ithibitike kuwa
hali hiyo ilitokea kabla au wakati wa kufunga ndoa na siyo baada ya kufunga
ndoa wakati kitendo cha kuitimiliza ndoa kilishafanyika. Ili ndoa iweze
kubatilika ni lazima kukosa nguvu huko kuthibitishwe na daktari kuwa hakuponi
au kunapona lakini mwanaume hataki matibabu. Mwanamke
anaweza kuwa na maumbile ambayo yanaweza kufanya ndoa
ishindwe kutimilizika. Ikithibitika hali hii inathibika lakini mwanamke hataki
tiba mwanamume anaweza kuomba mahakamani ndoa kubatilishwa. Ili mahakama iweze
kusikiliza shauri la kuomba kubatilisha ndoa ni lazima shauri hilo lipelekwe
haraka. Kama shauri litakwenda mahakamani baada ya mwaka mmoja tangu tarehe ya
ndoa Mahakama haitalipokea. Pia ni lazima ithibitike kuwa mlalamikaji alikuwa
hajui kasoro hiyo wakati wa kufunga ndoa na baada ya kuigundua hiyo kasoro
hajawahi kuingiliana na mwenzie mwenye kasoro hiyo.
Ndoa
batilifu huvunjwa na mahakama pekee baada ya kupokea malalamiko toka kwa mmoja
wa wanandoa. Kama hakutakuwa na malalamiko yatakayopelekwa mahakamani na
anayedhurika na kasoro hizo, ndoa hiyo itadumu ama labda mmoja afariki au kama
kuna talaka itatolewa na mahakama.
Watu
waliooana wana uhuru wa kugeuza ndoa yao kuwa ya mke mmoja au ya wake wengi
pale wanapofuata taratibu zinazokubalika kisheria. Kabla ya kufanya uamuzi wa
kugeuza ndoa ni budi wanandoa wakubaliane kuhusu uamuzi huo. Kitendo
cha kugeuza ndoa hufanywa mbele ya Hakimu wa Wilaya au Jaji
ambapo wanandoa watatoa tamko la maandishi lenye sahihi zao na Hakimu au Jaji
aliyeshuhudia naye hutia sahihi yake.
Katika
kugeuza ndoa, ndoa ya kiserikali ya kienyeji au ya Kiislamu inaweza kugeuzwa
kuwa ya mke mmoja kama kabla ya kugeuza hizi zinaweza kugeuzwa kuwa ya wake
wengi.
Ikumbukwe
kuwa kubadilisha dini pekee hakubadilishi hadhi ya ndoa. Vilevile ndoa ya
kikristo haiweza kugeuzwa kuwa ya wake wengi wala ndoa ya wake wengi inayodumu
kuwa ya mke mmoja.
SEHEMU YA NNE
TALAKA NA TARATIBU ZA
KE
Talaka ni ruhusa au amri ya
mahakama ya kisheria ambayo mume au mke hupewa wakati anapomwacha mwenzake.
Chombo
chenye mamlaka ya kutoa talaka ni mahakama tu. Mahakama hiyo itatoa talaka kwa
ndoa ambayo imedumu kwa muda wa miaka miwili au zaidi. Mahakama inaweza kutoa
talaka kwa ndoa ambayo haijafikisha muda huo endapo mlalalmikaji atatoa sababu
za msingi mahakamani.
KUTENGANA
Kutengana
si talaka. Kutengana maana yake ni hali ambayo mke na mume hukaa mbalimbali.
Kukaa mbalimbali au kutengana kwaweza kuwa kwa mapatano kati ya wanandoa hao au
kutengana kwaweza kuwa kwa amri ya mahakama. Mahakama itatoa amri hiyo endapo
mmoja wao atapeleka maombi mahakamani. Faida ya kutengana wote au mmoja wao
waweza au aweza kutambua makosa na baadaye kukata shauri kurudiana au kuishi
tena.
Kutengana
kwa mapatano, ni kutengana kwa hiari yao
wenyewe bila shuruti. Mapatano hayo yaweza 0
kuwa ya maandishi au ya mdomo. Mambo kadha yaweza
kuzingatiwa wakati wa makubaliano kama; heshima kwa kila mmoja, matumizi /
matunzo,watoto kama wapo watakaa na nani, mali ya pamoja je itatunzwa namna
gani na kutobughudhiana.
Kutengana
kwa amri ya mahakama, hii ni
hali ya mume na mke kutengana kwa amri ya mahakama na mahakama imeridhika kuwa
ndoa imevunjika. Ushahidi wa kuwa ndoa imevunjika ni ushahidi ambao unaweza
kutolewa mbele ya mahakama kunapokuwepo na maombi au shauri la talaka.
SABABU YA KUTOA TALAKA
MAHAKAMANI
Kabla ya
kupeleka shauri au maombi mahakamani ya talaka, mwanandoa husika hana budi
kufuata au kuzingatia hatua zifuatazo;
a)
kufungua au kupeleka malalamiko kwenye
Baraza la
Usuluhishi la Ndoa kwa mfano
Bakwata,
kanisani,Utawi wa Jamii au
Baraza la
Kata.
b) Baraza
litasikiliza, na endapo litashindwa
mapatano
au muafaka kati ya wanandoa hao,
basi baraza litatoa cheti ambacho kitaeleza kuwa
limeshindwa kusuluhisha mgogoro wa ndoa na kuomba
mahakama
kuendelea kutoa talaka.
c) Baada
ya mwanadoa mmoja kupata cheti hicho basi atatakiwa atayarishe madai ya talaka
akionyesha kuwa kulikuwa na ;-
ndoa
halali,
kuna
mgogoro kati yao,
watoto,
mali
walizochuma wakati wa ndoa yao,.
Muombaji huyo ataiomba
mahakama hiyo itoe amri ya
talaka,
mgawanyo
wa mali zilizochumwa kwa nguvu za pamoja,mamlaka ya kukaa na watoto na matunzo
yao,
gharama za madai / shauri.
Ili mahakama itoe talaka sababu
kadha huangaliwa na mahakama. Sababu hizo ni mambo ambayo yatakayofanya ndoa
ionekane kuwa imevunjika kiasi kwamba haiwezi kurekebishika tena, mambo hayo ni
kama ifuatavyo;
• • • • • • •
a) Ugoni;
hii ni zinaa ambayo hufanywa na mwanaume na mwanamke ambao hawajaoana.
Hii hutokea ambapo mwanaume ana mke wake
au mwanamke ana mume wake, hivyo mmoja wapo anamwacha mke/mume na kufanya zinaa
na mtu mwingine.
b) Ukatili; ukatili ni kuumiza
nafsi nyingine, kuharibu mwili au kuwa na hofu ya kuumizwa.
c) Kulawiti; kulawiti ni
kumwingilia mtu kinyume na maumbile,
d) Kichaa; ni kutokuwa na akili
timamu, na hali hii lazima iwe imethibitishwa na madaktari bingwa wa akili.
e) Kuzembea wajibu kwa makusudi;
haya ni majukumu ya mume, majukumu hayo ni kama haya; kumtunza mke kwa kumpa
chakula, malazi na mavazi.
f) Uasi Ni hali ya mke au mume
kuhama nyumba ya ndoa na kwenda kuishi mahala pengine bila sababu yoyote ya
msingi,
g) Kutengana; kukaa mbalimbali kwa
mume na mke kwa muda wa miaka isiyo pungua mitatu, kutengana kwao ni sababu
tosha ya talaka.
h) Dhana ya
kifo; hii ni hali ambayo mmoja wa wana ndoa amekufa, na hii hutokea iwapo
mojawapo hataonekana / ametoroka kwa muda mrefu, kama miaka 5. Hapo mahakama
hutoa tangazo kuwa fulani amekufa.
i) Kifungo; hii ni hali ambayo mume
au mke ametenda kosa la jinai na ametiwa hatiani na mahakama imemfunga miaka 5
au maisha basi mahakama inaweza kutoa talaka kwa mwombaji.
j) Tofauti za imani za kidini,
endapo mwanandoa mmoja atabadili dini basi ni sababu tosha ya kuomba mahakama
ivunje ndoa na kutoa talaka.
HAKI NA WAJIBU KATIKA NDOA
Baada ya kufunga ndoa na ikaonekana haina
kasoro yoyote, mke ana haki mbalimbali kisheria anazostahili kuzipata kisheria.
Haki hizi ni kama;
- Matunzo; mke au wake wana
haki ya kutunzwa na mume wao kwa kuwapatia mahitaji muhimu kama chakula,
malazi, mavazi, matibabu, n.k kulingana na uwezo alionao mume.
- Kumiliki mali; mke ana haki ya
kumiliki mali aliyoipata kabla na baada ya ndoa kama aliipata kwa
fedha yake
mwenyewe. Mke ana haki ya kuingia mikataba, kushitaki na kushitakiwa.
Makubaliano yaweza kufanywa na wanandoa hiyo jinsi ya kumiliki mali
iliyopatikana kabla ya ndoa yao jinsi gani waimiliki. Kwa mali iliyopatikana
wakati wa ndoa, mali hiyo ni mali ya wanandoa wote, kwa sababu imepatikana kwa
mchango wa nguvu za pamoja. Hii haijalishi kuwa mmoja wa wanandoa (mke)
hachangii pesa tasilimu au anakaa nyumbani na kufanya shughuli za nyumbani tu.
Kufanya shughuli za nyumbani ni mchango mkubwa na ameokoa fedha nyingi. Umiliki
wa mali kwa wanandoa haujalishi kuwa mmoja wapo amemiliki mali hiyo kwa jina
lake au la. Sheria ya Ardhi inatamka wazi kuwa kama mwanandoa mmoja anamiliki
mali kwa jina lake, na mwanandoa mwingine akachangia nguvu zake katika
kuendeleza, kuboresha au kuzalisha mali hiyo basi anapata haki ya kumiliki mali
hiyo.
- Haki ya kukopa kwa dhamana ya mume; jukumu la
kutunza mke na watoto ni jukumu la mume au baba. Kwa msingi huo, endapo baba
amesafiri, au ametoroka na baadaye matatizo yakajitokeza yanayohitaji fedha,
basi mke ana haki ya kukopa fedha kwa jina la mume au kuweka rehani mali ya
mumewe.
- Haki ya kuishi katika nyumba ya Ndoa;
Nyumba ya ndoa ni nyumba ambayo mke na
mume wanaishi wakati wa ndoa. Hata kama wanandoa wana nyumba nyingi, basi wanayoishi
au kutumia kama makazi ndiyo nyumba ya wanandoa. Nyumba hii haiwezi kuuzwa,
kuweka rehani au kuchukuliwa na mtu mwingine kama zawadi bila ya makubaliano ya
wanandoa wote.(bila ridhaa ya wanandoa). Mwanandoa ana haki ya kuishi kwenye
nyumba hiyo mpaka amri ya mahakama ya kuvunja ndoa, au kutengana itakapotolewa.
==========================
No comments:
Post a Comment